Ndugu
Wanahabari;
Mnamo Jumatatu
ya juma hili yaani siku ya Agusti 19, 2013 gazeti la Majira toleo Na: 7166,
gazeti la Jambo leo toleo Na: 1440, na gazeti la Mwananchi toleo Na: 4796 na
vyombo vingine vya habari viliripoti juu ya Mkutano wa baadhi ya Viongozi wa
Serikali za Wanafunzi wa Vyuo vya elimu ya juu hapa nchini uliofanyika mkoani
Morogoro. Mkutano huo uliwakutanisha baadhi ya Marais wa Serikali za Wanafunzi,
Makamu wa Rais wa Serikali za wanafunzi, Maspika wa mabunge ya Serikali za Wanafunzi,
na Viongozi waandamizi kutoka kwenye serikali mbambali za wanafunzi ambapo inasemekana
kuwa mkutano huo uliandaliwa na Taasisi ya kupambana na maadui watatu ambao ni
Ujinga, Maradhi, na Umaskini, inayofakamika kama FPID ambapo taasisi hiyo ina
makao yake makuu hapa Jijini Dar es Salaam.
Kwa Mujibu wa
taarifa za vyombo vya habari mkutano huo uliofanyika morogoro ulijadili masuala
ya utouti wa kipato kati ya watanzania, ubora wa elimu hasa maeneo ya vijijini,
na fursa za ajira. Lakini kubwa lililoibuka katika mkutano huu na kuchukua
uzito mkubwa wa Mkutano wenyewe ni suala la ‘ni nani awe Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mnamo Mwaka 2015’
Taarifa
Rasmi Kutoka TAHLISO.
Taasisi ya
Wanafunzi wa Vyuo Vya Elimu ya Juu imesikitishwa sana na inalaani vikali
matukio yaliyojitokeza katika Mkutano
huo kwani ni kinyume na maadili ya Elimu ya Juu hapa nchini. Watu wengi
wamehusisha Mkutano huo na taasisi yetu ya TAHLISO kwamba TAHLISO ndiyo
iliyoandaa Mkutano huo jambo ambalo sivyo.
Pamoja na hayo
TAHLISO inaarifu mambo yafuatayo kwa Umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwamba;-
- Mkutano Ulioitishwa Mkoani Morogoro ni batili na hautambuliki kwa mujibu wa sheria Na. 07 ya vyuo vikuu ya Mwaka 2005, sheria ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali Na. 24 ya Mwaka 2002 pamoja na Katiba ya TAHLISO.
- Shughuli za serikali za wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu ni kushuhulika na masuala ya wanafunzi na ubora wa taaluma itolewayo katika chuo husika na masuala mengine ya kitaifa lakini si kwa ushabiki wa kisiasa au kutetea kundi au maslahi ya watu fulani.
- Ni Jukumu la vyama vya siasa vilivyosajiliwa na kutambulika kiserikali kukaa na kuchagua au kuteua wajumbe wanaogombea nafasi mbalimbali za kisiasa iwe katika chama, serikali au vinginevyo lakini hilo siyo jukumu la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.
- Vikao vyote vinavyohusu mjumuiko wa serikali za wanafunzi vinapaswa kuitishwa na kuratibiwa na TAHLISO na siyo taasisi nyingine yeyote.
Hatua
zilizochukuliwa na TAHLISO kuhusiana na yaliyotokana na Mkutano wa baadhi wa Viongozi wa Serikali za
Wanafunzi Mkoani Morogoro.
- TAHLISO inatoa onyo kali kwa viongozi wa Serikali za Wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu ambao walishiriki kwenye Mkutano huo wa Morogoro kwamba wasirudie tena kufanya hivyo na vinara wa wanafunzi ambao walikuwa mstari wa mbele kuchochea masuala haya ya kisiasa bila ya kufuata utaratibu watawajibishwa ipasavyo.
- Ni marufuku kwa wanafunzi au makundi ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kuendesha harakati za siasa kwa kutumia jina la chuo, vyuo, au taasisi yoyote inayoshughulika na masuala la elimu ya juu hapa nchini.
- TAHLISO itawaandikia barua Waadili wote wa wanafunzi (Deans of Students) wa vyuo vya elimu ya juu na kuwapatia hadidu za rejea kuhusu utaratibu wa kubaini vikao halali na visivyo halali ili waweze kuratibu vyema ruhusa zitolewazo kwa viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kwa ajili ya kuhudhuria mikutano mbalimbali ambayo ipo nje na taratibu za chuo husika na inayohusiana na masuala ya wanafunzi kitaifa au vinginevyo.
- Kwa onyo hili la awali Viongozi wa Serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu watakaokiuka taratibu zilizoainishwa hapa watawajibishwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za adhabu zilizopo kwenye chuo husika.
Mwisho.
TAHLISO inawakumbusha wanafunzi wote wa elimu
ya juu nchini kwamba, jukumu lao ni kusoma na kujifunza taaluma zao kwa
taratibu zilizoanishwa na chuo husika. Hicho ndicho kilichowapeleka chuoni kwa
hiyo wafanye masomo kwanza, na chama chao ni taaluma, kisha siasa watafanya
baadaye.
Imetolewa na Ndg. Donati Primi Salla
Katibu Mkuu Mtendaji wa TAHLISO
No comments:
Post a Comment